Na: OWM-KAM, Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Mahusiano kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Bw. Rasheed Maftah, amesema Mwongozo wa Uratibu wa Mahusiano baina ya Serikali na Makundi ya Kijamii wa mwaka 2026 utakuwa daraja muhimu la mawasiliano na ushirikishwaji kati ya Serikali na makundi mbalimbali ya kijamii, kwa kuhakikisha maoni na sauti za wadau zinazingatiwa katika masuala ya kitaifa.
Amesema hayo leo, Agosti 18, 2026, wakati akifungua Warsha ya Kupokea Maoni ya Wadau kuhusu Rasimu ya Mwongozo huo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Bi. Mary Maganga, iliyofanyika Jijini Dar es Salaam.
Aidha, Bw. Maftah amesema kuwa mwongozo huo ni nyenzo muhimu wa kuimarisha uwazi, uwajibikaji wa pamoja katika uratibu wa mahusiano, huku ukichochea ushirikiano wa dhati baina ya Serikali na wadau kwa kuzingatia misingi ya usawa, maadili na mshikamano wa kitaifa.
“Kama mnavyofahamu, Novemba 2025, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ilipewa jukumu jipya la kuratibu suala la mahusiano baina ya Serikali na makundi ya kijamii, ikiwemo vyama vya siasa, taasisi za dini, mashirika yasiyo ya kiserikali na asasi za kiraia,” amesema Maftah.
Maftah ameeleza kuwa baada ya kupewa jukumu hilo, Ofisi imekutana na makundi mbalimbali kwa nyakati tofauti kwa lengo la kulitambulisha jukumu hilo, kuelimishana kuhusu dhana ya mahusiano na ushirikishwaji, pamoja na kupokea maoni kuhusu namna bora ya kuimarisha mahusiano baina ya Serikali na makundi ya kijamii. Maftah amesisitiza kuwa maoni hayo yamezingatiwa katika uandaaji wa rasimu ya mwongozo.
Hata hivyo, mwongozo huo si wa Serikali pekee, bali ni wa manufaa kwa makundi yote ya kijamii, yakiwemo vyama vya siasa, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za dini, asasi za kiraia, wazee, vijana, wanawake na makundi mengine muhimu katika jamii.
“Hivyo, ni wajibu wetu sote kushiriki katika kutoa maoni, ushauri na mapendekezo yatakayoboresha mwongozo huu na kuhakikisha unatekelezwa kwa vitendo kwa ajili ya manufaa ya taifa letu,”
Wakitoa maoni mbalimbali, Katibu Mkuu wa Baraza la Kitaifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Bi. Fransisca Mboya, ameishukuru Serikali kwa kuwashirikisha wadau katika mchakato wa kuandaa mwongozo huo, akisema umeandaliwa vizuri na umezingatia ushirikishwaji wa makundi katika ngazi mbalimbali.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Bw. Salehe Abdallah, amesema mwongozo huo utasaidia kuimarisha ushirikishwaji katika uendeshaji wa Serikali na michakato ya kufanya maamuzi.
Naye, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani, Dkt. Isaya Mgalagu, amesema kazi kubwa imefanyika katika kuandaa mwongozo huo, akieleza kuwa unagusa ngazi mbalimbali za jamii kuanzia ngazi ya kitaifa hadi ngazi ya chini.
Ameongeza kuwa ushirikishwaji huo utasaidia kujenga taifa lenye umoja, upendo na mshikamano, akisisitiza kuwa wananchi wanapokuwa na mshikamano, huwa sehemu muhimu ya kulinda amani na usalama wa nchi.

.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
Comments
Post a Comment